MAKALA

Siasa zinavyoua soka la zanzibar


Na, Ally Mohamed, Zanzibar

Mwanzoni mwa mwezi disemba mwaka 2014, Chama cha Mpira wa Miguu Visiwani Zanzibar (ZFA), kiliitisha mkutano mkuu wa kawaida, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Judo, Amani, Mjini Unguja.

Ilikuwa ni mkutano uliohudhuriwa na viongozi wote wakuu pamoja na wajumbe karibu wote ukiwa na lengo la kujadili kile kilichoitwa "rasimu" na hatimae kupitisha katiba mpya ya chama hicho.

Hata hivyo, wakati mkutano ukiendelea kujadili rasimu ya katiba mpya ya ZFA, ndipo aliponyanyuka Makamu wa Rais wa ZFA upande wa Unguja, Haji Ameir Haji (Mpakia), na kupingana na viongozi na wajumbe wa mkutano huo kwa mambo mawili.

Moja, alisema mkutano huo si halali kwa mujibu wa katiba ya ZFA, pili alisema rasimu inayojadiliwa si halali huku akijenga hoja kuu mbili kuhusu rasimu hiyo, moja ni; rasimu iliyokuwa ikijadiliwa ni mbovu kuliko hata hiyo katiba inayotaka kubadilishwa, pili kabla ya mkutano mkuu wa ZFA Taifa ni sharti rasimu hiyo irudi kwa wadau (wachezaji wa zamani, vilabu vya mpira wa miguu, Baraza la Michezo Zanzibar) ili watoe maoni yao katika rasimu hiyo na kisha mkutano utakaoitishwa tena uwe ni kwa ajili ya kupitia maoni ya wadau kuhusu rasimu ya mabadiliko ya katiba ya ZFA.

Hata hivyo, mkutano huo haukumalizika kwa afya nzuri, kwani kilichotokea hapo ni kuanza kurushiana maneno makali kati ya viongozi na wajumbe dhidi ya Makamu wa Rais wa ZFA (Unguja), na hatimae makamu huyo akatoka katika mkutano huo na kusema anakwenda kufanya mambo mawili,
Moja ni kumuandikia barua Mrajis wa Vyama vya Michezo Zanzibar, akimtaka azuie mkutano huo kuendelea na pia azuie kujadiliwa kwa rasimu ya katiba, pili kama itashindikana Mrajis kuchukuwa hatua hiyo basi angekwenda mahakamani kupinga hatua zozote zitakazoamuliwa na mkutano huo.

Kweli, aliandika barua kwenda kwa Mrajis wa vyama vya michezo na baada ya kutokujibiwa kwa barua hiyo hatimae tarehe 12 disemba 2014, akaamua kwenda Mahakama Kuu ya Zanzibar kufungua shauri la kutaka kuzuiwa kufanya shughuli zao viongozi wakuu watatu wa ZFA. Viongozi hao ni Rais wa ZFA Taifa, Ravia Idarous Faina, Makamu wa Rais wa ZFA (Pemba) Ali Mohammed na Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji Salum.

Shauri jengine ilikuwa ni matumizi mabaya ya ofisi na kuzuia hatua za kupatikana katiba mpya ya ZFA. Mahakama Kuu ya Zanzibar ikatoa muongozo wa shauri hilo tarehe 16 disemba 2014 kwamba Rais wa ZFA, Makamu wake kutoka Pemba na Katibu Mkuu wa ZFA hawaruhusiwi kujishughulisha na utendaji wowote ndani ya taasisi hiyo mpaka pale shauri lililofunguliwa mahakamani litakapoamuliwa.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama Zanzibar ikalazimika kusimama kwa shughuli zote za mpira wa miguu hali ambayo inatajwa pia kuwa sababu iliyochangia kukosekana kwa wadhamini katika soka la Zanzibar ambalo linaendeshwa kwa kuchanganya siasa za 'U-unguja' na 'U-pemba', 'U-CCM' na 'U-CUF'.

Tarehe 24 disemba 2014, Mahakama Kuu ya Zanzibar ikatoa muongozo na kulegeza masharti na kuamua kuwa, shughuli za mpira wa miguu ziendelee kwa kuundwa kamati ya mpito itakayosimamia shughuli zote za mpira wa miguu isipokuwa hawatakuwa na mamlaka ya kuitisha uchaguzi, kubadili katiba na pia watatakiwa kufanya ukaguzi wa hesabu kwa kutumia muhasibu kutoka nje ya taasisi ya ZFA. Sanjari na hilo tarehe 31 disemba 2014 Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar (BTMZ) nao wakatoa muongo unaofanana na huo.

Barua ya Baraza la Michezo la Taifa la Zanzibar iliyokuwa na kumbukumbu namba; BTMZ/MR/VOL.11/07, alipelekewa Katibu Mkuu ZFA Taifa ikiwa na kichwa cha habari "KUH: KUFUTA BARUA YA TAREHE 10/12/2014 na kumuamuru kufanya mambo yafuatayo;

-Kufanya marekebisho yote ya Katiba kama alivyoagizwa kulingana na barua ya awali kwa mujibu wa FIFA Standard Statutes.
-Kuirejesha tena Katiba hiyo kwenye mkutano mkuu kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu. 
-Kusitisha shughuli zote za uchaguzi mpaka pale katiba itakaporekebishwa. Barua hiyo ilikuwa na msisitizo kuwa hayo maelezo hayakuwa ombi bali ni AMRI na iliandikwa na kusainiwa na Mrajis wa vyama vya michezo Zanzibar, Said M. Juma.

Baada ya hapo siasa zikapita na kuletewa 'mazingaombwe' kuwa kesi imeondolewa mahakamani, nasema ni mazingaombwe kwa sababu wahusika hawakuja na ushahidi wowote kutoka mahakamani ulioonesha kuwa kesi hiyo imefutwa, zaidi wahusika walitaka kuhalalisha Mashindano ya kombe la Mapinduzi 2015.
Kweli baada ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, mgogoro ukaibuka tena mahakamani kwamba hakukuwa na kesi yeyote iliyofutwa zaidi ya kuendekeza siasa za kufurahishana, mgogoro ulipokuwa mkubwa mahakama ikatoa muongozo mwengine wa kuwazuia wote waliofungua shauri na waliofunguliwa wasijishughulishe na uongozi katika soka la Zanzibar.

Kufuatia hali hiyo, ndipo Kamati Maalum ikakutana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), kwa lengo ka kutafuta muafaka, baada ya majadiliano ikakubaliwa mambo yafuatayo yafanyike ili kulinusuru soka la Zanzibar.

Moja; kujadili mwenendo wa Kamati Tendaji ya ZFA, mbili; kuteua mkaguzi wa mahesabu kukagua vitabu vya mahesabu ya ZFA na tatu kuteua Kamati Maalum ya kuandika upya katiba ya ZFA.

Itakumbukwa kuwa katika amri ya Mahakama Kuu iliyotolewa siku ya tarehe 16 disemba 2014 na ile ya tarehe 24 disemba 2014 katika kesi namba 62/2014 lakini pia barua ya Serikali kupitia Mrajis wa vyama vya michezo ya tarehe 31 disemba 2014 zote kwa pamoja zulizuia kufanyika baadhi ya shughuli ikiwemo uchaguzi ingawa kuna chaguzi zilifanyika kwa mantiki ya barua ya mahakama na ya Mrajis chaguzi zote zilizofanyika ni batili.

Wakati hayo yakiendelea ghafla tukasikia ZFA imeamua kufanya Mkutano Mkuu wa Dharura ukiwa na ajenda tatu, mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Kikwajuni, Mjini Unguja, wiki iliyopita. Ajenda ya kwanza ni kujadili mwenendo wa kamati tendaji ya ZFA, ajenda ya pili ni kuhusu kuteuliwa Mkaguzi wa Mahesabu kwa ajili ya kuvipitia vitabu vya mahesabu vya ZFA.

Na ajenda ya tatu ni Mkutano Mkuu ulikuwa unatakiwa kuamua kuteuwa wajumbe 5 watakaoandika upya Katiba ya ZFA.

Maamuzi haya yamefanywa na ZFA kihuni kwa sababu hayakuzingatia muongozo wa mahakama wala makubaliano ya viongozi wa ZFA na TFF, ni dhahiri kuna kikundi cha watu wachache ambao naamini wanapata nguvu kutoka kwa viongozi wa Serikali kufanya uhuni huu.

Haiwezekani kufanya maamuzi ambayo yanakinzana na amri ya mahakama halafu watu hao wanaangaliwa tu kama vile nchi haina mihimili yenye mamlaka, kwa mfano katika mkutano huo batili wa dharura wajumbe kwa wingi wao walipiga kura ya kumsimamisha Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, wakaivunja Kamati ya Muda ya ZFA ambayo ipo kwa muongozo wa nahakama na ofisi ya Mrajis kama vile haitoshi wakatangaza kuwa chaguzi zote zilizofanyika wakati wa zuio la mahakama (court junction) ni sahihi na wanazitambua kama huu si uhuni tuuwiteje?

Ni bahati mbaya sana siasa zimetumika kutufikisha hapa lilipo soka la Zanzibar, viongozi wetu hawana habari yeyote na michezo licha ya kuwa kuna Wizara inayoshughulikia michezo, hawana kazi wanayofanya kulinusuru soka la Zanzibar badala yake kila mmoja anafanya anavyotaka.

Hivi ni nani aliyeturoga lakini? Mbona kuna mambo yanakwenda kama vile hakuna viongozi, yote haya katika soka la Zanzibar viongozi wa Wizara husika hakuna hatua yeyote waliyoichukuwa wala kupaza sauti zao nadhani wala hawana habari nayo.

Najiuliza hivi vile vikao walivyofanya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk na makongamano ya kutosha kuhusu soka letu haya yote yalikuwa na maana gani? Nauliza hivyo kwa sababu hakuna hata moja lililofanyiwa kazi zaidi ya porojo zisizo na tija yeyote. Labda faida ya posho, vinywaji na vitafunwa kwa wingi.
Binafsi sijaona umuhimu wowote wa kuwa na Wizara inayosimamia michezo kwa Zanzibar, sasa hivi Zanzibar inategemea Mashindano ya Kombe la Mapinduzi tu baada ya hapo hakuna soka hii ni aibu ya karne na hata hayo Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanategemea uwepo wa Timu za Simba na Yanga tu zikikosekana mashindano yote yanapooza.

Hivi tutaendelea kutegemea Kombe la Mapinduzi mpaka lini? Ni viongozi wa aina gani tulionao ambao hawajui wajibu wao kiasi hiki katika kutekeleza majukumu yao? Viongozi wa aina hii wana faida gani? Ligi Kuu ya Zanzibar inachezwa kwa mafungu mara utasikia ligi kuu kanda ya Unguja mara ligi kuu kanda ya Pemba kuna timu ipo Unguja ila mpaka leo imegoma kucheza ligi, ligi haina mdhamini hata wa kubahatisha, gharama za kujiendesha vilabu ni kubwa, vilabu vinashiriki ligi ambayo haina zawadi kwa bingwa wala makamo bingwa utajiuliza hivi vilabu vyetu vinagombea nini katika hiyo inayoitwa ligi kuu ya 'mafungu'?
Hakuna malaika atakayeshuka kuja kutuendeshea mpira wetu ni sisi wenye kuamua kubadilika kwa kufanya kazi tukiongozwa na udhati wa nafsi zetu badala ya kusukumwa na maslahi binafsi na kuwaumiza wengine, viongozi wa sasa wa ZFA wamekosa sifa na uhalali wa kuhudumu katika taasisi hiyo na ni busara kwao wakakaa pembeni kuwapisha wenye uchungu na soka la Visiwa hivi kuja kulifufua maana wao tayari walikwashalizika na kuendelea kuwapa muda ni kuzidi kulisahaulisha milele.