Sunday 28 February 2016

Makonda: Walimu bure kusafiri Dar

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA), Sabri Mabrouk na Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Daladala (Uwadar), William Masanja, kulia. 



Pengine hii yaweza kuwa ni historia; kuanzia Machi 7 walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaofundisha shule za Serikali za msingi na sekondari, hawatalipa nauli kwenye kwenye daladala wakati wakienda na kutoka kazini.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitangaza hayo jana mbele ya viongozi wa vyama vya usafirishaji abiria na madereva Mkoa wa Dar es Salaam.

Makonda alisema wazo lake la kutaka walimu wasafiri bure limeungwa mkono na viongozi wa vyama vya wasafirishaji abiria na wamiliki wa daladala na kwamba kilichobaki ni kuanza kutoa huduma hiyo.

“Awali, wazo langu ilikuwa walimu wa Wilaya ya Kinondoni ninayoiongoza, ndiyo wafanyiwe utaratibu wa kusafiri bure lakini wadau wa usafirishaji wakashauri iwe kwa mkoa mzima. Nikamweleza mkuu wa mkoa na akaniruhusu tufanye hivyo mkoa mzima,” alisema Makonda ambaye mpango wake wa kuchangia ujenzi wa shule umemhakikishia cheo baada ya Rais John Magufuli kuguswa.

Makonda alisema kuanzia leo, wakuu wa shule za msingi watakakiwa kuwatengenezea walimu wao vitambulisho kwa ajili ya usafiri.

Alisema vitambulisho hivyo ambavyo vitavaliwa wakati wa kupanda daladala, vitatakiwa kuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili na jina la shule anayofundisha.

Mkuu wa wilaya hiyo alisema vitu vingine vinavyotakiwa kuwa kwenye vitambulisho hivyo ni saini ya Makonda ili kuepuka udanganyifu na namba ya simu ya mkuu wa shule husika.

Alisema baada ya vitambulisho kukamilika, walimu watapanda bure katika daladala lolote wakati wa kwenda kazini kuanzia saa 11.30 hadi saa 2.00 asubuhi na kwamba wakati wanarejea nyumbani huduma hiyo itaanza saa 9.00 alasiri hadi saa 11.00 jioni.

Makonda alisema huduma hiyo ya usafiri bure kwa walimu itatolewa siku tano kwa wiki kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa na kwamba siku za Jumamosi, Jumapili na sikukuu watatakiwa kulipia.

“Huo ni muda ambao wamiliki wamekubali kusafirisha walimu bure kwenda kazini na kurudi nyumbani. Nje ya muda huo walimu watatakiwa kulipa nauli kama kawaida,” alisema.

Makonda alisema baada ya Rais Magufuli kutangaza elimu bure, aliona amuunge mkono kwa kuweka mazingira yatakayorahisisha utendaji kazi wa walimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala cha Dar es Salaam (Darcoba), Sabri Mabruki alisema wamekubali kutoa usafiri bure kwa walimu ili kumuunga mkono Magufuli katika juhudi zake za kuboresha elimu. “Tumeletewa ombi na mkuu wa wilaya akitueleza kuhusu wazo la kutaka kusafirisha walimu bure. Kwa namna Makonda na Rais wanavyofanya kazi, hatukuwa na kinyongo zaidi ya kukubali ombi hilo,” alisema.

Akiunga mkono huduma hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria (Uwadar), William Masanja alisema elimu bure haiwezi kufanikiwa kama mazingira ya kazi ya walimu yatakuwa magumu.

“Ndiyo maana tulivyoambiwa na mkuu wetu wa wilaya, hatukuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kukubali ombi lake. Tumejipanga kuwasafirisha walimu ili waweze kufundisha watoto wetu,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Shaaban Mdemu aliwataka walimu kuzingatia muda uliopangwa kusafiri bure ili kuondoa usumbufu.

Aliwataka wamiliki wa daladala kuwa wasikivu iwapo wataambiwa na madereva wao kuwa mapato ya siku yamepungua kutokana na kuwepo kwa huduma hiyo.

Akizungumzia uamuzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch alisema jambo hilo likitekelezeka, Makonda atakuwa kiongozi wa mfano hapa nchini kuthamini kazi za walimu.

“Mpango huu unatakiwa kupongezwa, kuungwa mkono na wadau wa elimu. Tunahitaji kuwapa moyo viongozi wabunifu kama hawa,” alisema.

Alisema walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanatumia wastani wa Sh3,000 kwa siku kwa ajili ya usafiri wa daladala.

“Sehemu kubwa ya mishahara ya walimu inatumiwa kwa ajili ya usafiri, mpango huu utakuwa mkombozi kwao,” alisema.

Alisema kama mpango huo utafanikiwa mkoani Dar es Salaam, unatakiwa kuanzishwa kote nchini.

Hata hivyo, Oluoch alipendekeza mpango huo utungiwe kanuni ili makubaliano hayo yaendelee kudumu hata kama viongozi hao hawatakuwepo Dar

No comments: