Monday 29 February 2016

Mbowe akosoa operesheni tumbua majipu

Mwenyekiti wa CHADEMA na Mbunge wa Hai Mh. (mb) Freeman Mbowe (picha na Maktaba)

Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), amekemea kile alichokiita “fukuza fukuza” ya watumishi wa umma bila kufuata taratibu.

Kauli ya Mbowe imekuja wakati Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, ikiwa katika kampeni ya kufukuza na kusimamisha watumishi wa umma wanaotuhumiwa kuhusika katika ubadhirifu, wizi, uzembe na njama za kuhujumu mapato.

Operesheni hiyo inafanyika kwa kuwasimamisha kazi watumishi hao huku uchunguzi ukiagizwa kufanywa wakati tuhuma zao zikiwa zimeshatajwa hadharani.

Tayari watumishi zaidi ya 160 wameshasimamishwa au kufukuzwa kazi tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Kati yao, tayari wachache wamefikishwa mahakamani.

Mbowe alisema ufukuzaji watumishi wa umma bila ya kufuata taratibu hautakiwi na kuwataka viongozi wa dini kukemea mwenendo huo.

Alitoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo katika ibada maalumu iliyofanyika kwenye usharika wa Nshara wilayani Hai.

Ibada hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, ilikuwa ni kwa ajili ya uzinduzi wa ukarabati na upanuzi wa jengo la Kanisa la Bethel lililopo katika Usharika wa Nshara.

Mbowe alisema hadi sasa, zaidi ya watumishi 160 wa Serikali wamefukuzwa au kusimamishwa kazi bila Serikali kuweka wazi makosa yao, huku familia za baadhi yao zikiendelea kutaabika.

Mbali na suala hilo, aliwataka viongozi wa dini kuingilia kati mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar ambako alisema dhana ya demokrasia haifuatwi kama viongozi wa Serikali wanavyodai.

Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Shoo hakujikita kuzungumzia suala hilo, badala yake alijielekeza zaidi kwenye uharibifu wa mazingira.

Askofu Shoo alisema licha ya Tanzania kuwa na Sheria nzuri za kudhibiti mazingira, hazifuatwi hali inayosababisha asilimia 60 ya eneo la nchi kuwa jangwa.

Askofu alisema kutofuatwa kwa sheria hizo kumesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kusababisha majanga kwa baadhi ya maeneo yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Dk Shoo alisema kumekuwapo na mafuriko ya mara kwa mara, kutokana na wananchi kutozingatia kilimo bora hali inayosababisha mmomonyoko wa ardhi, ikiwa ni pamoja na ardhi kupoteza rutuba.

“Wananchi wamekuwa wakitumia sumu katika vyanzo vya maji hali inayosababisha vyanzo vingi kukauka na Kilimanjaro ni miongoni ya maeneo ambayo yanatajwa kuwa jangwa,” alisema Askofu Shoo.

Askofu Shoo alisema tafiti mbalimbali na zinaonyesha ukataji wa misitu umesababisha uharibifu mkubwa hivyo ni vyema Serikali ikachukua hatua za haraka ili kuokoa kizazi kijacho.

Aliwataka wananchi kuchukua hatua za haraka kutunza mazingira hususan miti ya asili ambayo inaweza kusaidia kurudisha uoto wa asili ambao tayari umeharibiwa baadhi ya maeneo.

Katibu wa kamati ya ukarabati na upanuzi wa kanisa hilo, Endrey Uronu, alisema zaidi ya Sh1.5 bilioni zinahitajika katika ujenzi huo huku katika harambee iliyofanyika jana, Sh279 milioni zilipatikana.

No comments: