Wednesday 16 March 2016

Mtoto Mchanga aibiwa Wodini katika hospitali ya Mkoa wa Arusha


Hali ya sintofahamu imeibuka katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru baada ya mtoto mchanga wa siku tano kuibiwa wodini katika mazingira ya kutatanisha.

Tukio hilo limezusha hofu kwa baadhi ya wazazi waliojifungua katika wodi ya wazazi hospitalini hapo wakihofia usalama wa watoto wao na kuomba Serikali kuingilia kati.

Akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mtoto huyo, Sinyari Lucas ambaye ni mkazi wa Simanjiro mkoani Manyara, amesema limetokea usiku wakuamkia jana.

Akizungumza huku akiwa ameghubikwa na huzuni, Bi Sinyari
amesema wakati akiwa kitandani muda wote kabla ya kulala alikuwa na mtoto wake.

Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Jackline Urio amekiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba, uongozi umelipokea kwa mshtuko mkubwa na unalifanyia kazi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amesema wamepokea taarifa hizo na tayari ameagiza maofisa kwenda kufuatilia tukio hilo kwa kina.